Somalia iko katika mtafaruku wa kikatiba:UM

30 Machi 2011

Serikali ya mpito ya Somalia ambayo ina matatizo ya kukabiliana na wanamgambo wa Kiislaam wenye uhusiano na Al-Qaeida sasa inakabiliwa na matatizo mengine ya kikatiba ambayo yanatishia kusambaratisha juhudi za usalama zilizoaanza kuonekana.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Balozi Augustine Mahiga amesema mtafaruku huo umezuka baada ya juhudi za bunge na serikali kuongeza muda wake na kwamba jumuiya ya kimataifa haikubaliani na sabu zilizotolewa za serikali kuongeza muda baada ya muda wa mwisho wa kumalizika serikali hiyo hapo mwezi Agosti.

Nchi hiyo imekuwa katika vita kwa miongo miwili sasa, huduma muhimu hazipatikani na wakazi mara nyingi wanajikuta katikati ya mapigano kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo. Mwezi Februari bunge la nchi hiyo lenye wabunge 550 liliamua kujiongezea muda wa miaka mitatu suala lililokosolewa vikali na wahisani wakiwemo Marekani.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud