Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Yemen yanazidisha adha kwa maelfu ya watu:Amos

Mapigano Yemen yanazidisha adha kwa maelfu ya watu:Amos

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa leo ameonya kwamba mapigano yanayoendelea Yemen yanazidisha adha kwa hali ambayo tayari ni mbaya, na amezitaka pande zote kusitisha machafuko.

Inakadiriwa kwamba machafuko ya Yemen ambayo ni sehemu ya maandamano yaliyoghubika Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini yameshakatili maisha ya watu 82 na kujeruhi wengine wengi. Maandamano yao ni ya kutaka mabadiliko ya kiuchumi, kidemokrasia na kijamii.

Valarie Amos amesema anahofia kuhusu hali ya kibinadamu Yemen kwa sababu hata kabla ya maandamano haya nchi hiyo ilikuwa inakabiliwa matatizo ya kibinadamu kutokana na machafuko ya Kaskazini mwa nchi hiyo yaliyosababisha watu 300,000 kukimbia nyumba zao.

Kwa mujibu wa OCHA nchi hiyo pia inakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula na maji huku watu milioni 2.7 sawa na asilimi 31.5 ya watu wote hawana chakula cha kutosha.

Bi Amos pia amesema baadhi ya mashirika ya misaada yanakabiliwa na vizingiti kuweza kuwafikia maelfu ya watu wanaohitaji msaada. Amesema hivi sasa Umoja wa Mataifa unajadiliana na serikali na waasi wa Al-Houthi ili kutatua hali hiyo.