UM/AU wasema vijiji vimetelekezwa Darfur baada ya mapigano

UM/AU wasema vijiji vimetelekezwa Darfur baada ya mapigano

Mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika, umebaini kwamba vijiji kadhaa Kaskazini mwa Darfur Sudan eneo vilivyoshuhudia mapigano makali mapema mwezi huu baina ya majeshi ya serikali na waasi vimetelekezwa.

Takribani vijiji viwili kati ya vitano vilivyo kilometa 15 hadi 30 mwaka Shangil Tobaya vimetelekezwa kabisaa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa na ule wa Afrika wa kulinda amani Darfur UNAMID.

UNAMID imesema wakazi wa vijiji hivyo vitano ni miongoni mwa watu 70,000 waliosambaratishwa na mapigano hayo ya mwanzoni mwa mwezi huu. Timu ya kupata ukweli iliyoongonzwa na ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA, UNAMID na tume ya msaada wa kibinadamu Kaskazini mwa Darfur pia, imebaini mabaki mengi ya silaha.

Tume hiyo ina mpango wa kurejea tena siku zijazo kufanya uchunguzi zaidi. Tume hiyo ilianzishwa mika mitatu iliyopita ili kufuatilia ghasia za Darfur ambako watu wapatao 300,000 wameuawa na wengine milioni 2.7 wamelazimika kuzikimbia nyumba zao kutokana na mapigano.