Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mionzi iliyosambaa nje ya Japan sio tishio:WHO

Mionzi iliyosambaa nje ya Japan sio tishio:WHO

Mionzi hivi sasa inasafiri kutoka katika kinu cha nyuklia cha Japan kilichoharibiwa na tetemeko na tsunami kwenda katika nchi zingine, lakini shirika la afya duniani WHO linasema mionzi hiyo ya nje sio tishio.

Kumekuwa na utata mkubwa juu ya kiwango gani cha mionzi kinavuja na kusafiri hewani. Msemaji wa Who Gregory Hartl amesema kuna mashirika mbalimbali na serikali duniani kote zinazopima kiwango cha mionzi hali ambayo inaweza kuleta taarifa tofauti. Amesema WHO inafahamu hali ni nyeti lakini hatutaki kuwakanganya watu , Who inarejea kusema kwamba kwa wakati huu mionzi iliyotoka nje ya Japan sio tishio kwa afya ya jamii.

Wakati huohuo wafanyakazi watatu wa mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daiichi walipatwa na kiwango kikubwa cha mionzi siku ya Alhamisi baada ya kusimama kwenye maji yaliyoathiriwa na mionzi hiyo. Shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA linasema hadi sasa wafanyakazi 17 wameathirika na kiwango Fulani cha mionzi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito ambao pia umetolewa na IAEA wa kufanyika tathimini ya hatua za usalama kwa vinu vyote vya nyuklia baada ya kuzuka tafrani hii. Maafisa wa serikali ya Japan wametangaza kwamba wamepitia upya idadi ya waliokufa kwenye tsunami na tetemeko la Machi 11 na sasa idadi imefika 10,000 na wengine wengi bado hawajulikani waliko.