Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

serikali zimetakiwa kutimiza makubaliano ya Cancun:UNFCCC

serikali zimetakiwa kutimiza makubaliano ya Cancun:UNFCCC

Ikiwa ni chini ya wiki mbili kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa mjini Bangkok hapo Aprili 3 hadi 8 mwaka huu, afisa wa Umoja wa mataifa amezitaka serikali kuongeza kasi ya kutimiza kwa wakati makubaliano ya Cancun ya Desemba 2010.

Christiana Figueres katibu mkuu wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa UNFCCC amesema dunia ilikuwa njia panda Cancun na ikachukua hatua ya kusonga mbele kuwa na dunia yenye mazingira salama.

Ameongeza kuwa sasa serikali ni lazima zifuate njia zilizoweka na kushikilia kasi waliyonayo kwenye mkutano ujao wa Bankok ili kuweza kuchukua hatua kubwa zaidi ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa mjini Durban Afrika ya Kusini mwishoni mwa mwaka.

Bi Figueres ameyasema hayo kwenye mkutano wa mawaziri mjini Mexico City ambao wanajadili utekelezaji wa makubaliano ya Cancun na mkutano ujao wa Thailand ambao utakuwa ni wa kwanza kwa serikali kukutana baada ya Cancun ili kusukuma mbele malengo waliyokubaliana.