Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yaomba msaada wa wahandisi wa kijeshi kusaidia huduma muhimu

Somalia yaomba msaada wa wahandisi wa kijeshi kusaidia huduma muhimu

Waziri wa mambo ya ndani wa Somalia Zahra Ali Samantar amewaomba wahandisi wa kijeshi kusidia nchi yake kufikisha huduma muhimu kwa watu.

Akizungumza kwenye baraza la haki za binadamu mjini Geneva hii leo ameomba msaada kwa ajili ya serikali ya mpito ya Somalia na vikosi vya kulinda amani vya muungano wa Afrika AMISON Bi Samantar amesema msaada huo unahitajika sana kwenye eneo la Kusini na Katikati mwa Somalia ili kuondoa ajenda za kisiasa za wanamgambo wa Kiislam wenye itikadi kali.

Amesema msaada huo wa wahandisi ni muhimu sana kuweza kuteka mioyo na imani za vijana hasa kwa kuwafikishia huduma za kijamii, kiuchumi na maendeleo.

Somalia bado inahangaika kuweza kuunda taasisi za serikali baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya zaidi ya miongo miwili vilivyochagia kutokuwa na serikali kuu. Zaidi ya Wasomali nusu milioni ni wakimbizi katika nchi jirani huku maelfu kwa maelfu wengine wakisalia kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na vita na ukame.