Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzalishaji wa ngano kuongezeka duniani 2011:FAO

Uzalishaji wa ngano kuongezeka duniani 2011:FAO

Utabiri wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO unaonyesha uzalishaji wa ngano duniani kwa mwaka huu 2011 ni tani milioni 676 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.4 ikilinganishwa na mwaka 2010.

Mafanikio hayo yametolewa leo katika ripoti ya FAO ya matarajio na hali ya chakula kwa mwaka 2011. Kilimo cha ngano kimepanda katika nchi nyingi kutokana na bei nzuri ya zao hilo, na hata kwenye maeneo yaliyokabiliwa na ukame kama Urusi hali imeenza kutengamaa. George Njogopa anayo ripoti kamili.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Hata hivyo ripoti hiyo ya FAO imesema kuwa bado ni mapema mno kubashiri moja kwa moja namna uzalishaji wa mazao hayo utakayojitokeza kwa mwaka huu kwani baadhi ya maeneo bado hayajanza kilimo. FAO imesema kuwa kuna ishara kubwa ya kuimarika kwa hali ya chakula hata kwenye maeneo yanayotambulika kuwa na  kipato cha hali ya chini, jambo ambalo ni ishara  ya kutia matumaini.

Kuna nchi kadhaa zimetajwa ambazo zinatazamiwa kuvuna kwa wingi wakati wa msimu wa uvunaji ikiwemo nchi zilizoko kwenye eneo la afrika ya kaskazini, isipokuwa tu kwa Tunisia ambayo mavuno yake yanategemewa kuyumba. Afrika Kusin pia ni miongoni mwa maeneo ambayo yanayotegemewa kuwa na mavuno mazuri ya mahindi kama ilivyo kwa nchi za Malawi na Zambia.