Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvumbuzi wahitajika kukidhi mahitaji ya maji mijini:FAO

Uvumbuzi wahitajika kukidhi mahitaji ya maji mijini:FAO

Shirika la kilimo na mazao la Umoja wa Mataifa FAO linasema kuwa kunahitajika kufanyika uvumbuzi mpya ili kuhakikisha kuwa kuna maji ya kutosha na salama kwa wanaoishi mijini kwenye nchi zinazoendelea wakati kunapoendelea kushuhudiwa kuongezeka kwa watu kwenye sehemu za miji.

Naibu katibu mkuu anayehusika na masuala ya mali asili kwenye shirika la FAO Alexander Mueller anasema kuwa kwa miaka 20 inayokuja asilimia 60 ya watu wote duniani watakuwa wakiishi mijini hususan kwenye mataifa yanayoendelea.

Mueller anasema kuwa kuwahakikishia watu hawa chakula nafuu hususan kwa wale maskini itakuwa changamoto kubwa. Nchi zinazoendelea nyingi hadi sasa zinakabiliwa na matatizo ya maji. Je wakazi hawa wa Afrika ya mashariki wanasemaje?

(MAONI KUHUSU SIKU YA MAJI)

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akitoa ujumbe maalumu kuhusu siku hii ya maji duniani amesema bila maji hakuna utu na hakuna kuepuka umasikini. Amesema maji ni bidhaa muhimu yenye uhusiano wa karibu na chakula na nishati na upungufu wa maji ni moja ya changamoto kubwa zinazoikabili dunia hivi sasa.