Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya ICC yataja tarehe mpya ya kuanza kesi ya vigogo wa Kenya

Mahakama ya ICC yataja tarehe mpya ya kuanza kesi ya vigogo wa Kenya

Kitengo cha kesi cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC leo kimetangaza tarehe mpya ya kuanza kusikiliza kesi ya vigogo wa Kenya wanaoshutumiwa kwa kuhusika na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu 2007.

Kesi dhidi ya Francis Kirimi Muthaura, Uhuru Muigai Kenyatta na Mohammed Hussein Ali sasa itaanza Aprili 8 2011 mchana mjini Hague badala ya tarehe 7 Aprili 2011 iliyotangazwa awali.

Katika uamuzi wake mahakama imesema mabadiliko haya ya tarehe yanatokana na ukweli kwamba tarehe 7 April majira ya mchana mahakama itakuwa na shughuli za kesi zingine zinazoendelea.

Hata hivyo tarehe ya kupanda mahakamani kuanza kusikilizwa kesi za washutumiwa William Samoei Ruto, Henry Kiprono Kosgey na Joshua Arap Sang inasalia kuwa April 7 2011 majira ya asubuhi saa za Hague.

Kenya iliridhia mkataba wa Roma tarehe 15 Machi 2005 na kuwa nchi mwanachama wa mahakama hiyo.

Machi 8 mwaka huu ICC ilitoa taarifa ya kuwaita mahakamani maafisa hao sita wa serikali ya Kenya kujibu tuhuma dhidi yao za kushiriki machafuko ya baada ya uchaguzi yaliyowaacha watu zaidi ya 1000 wakipoteza maisha na wengine wengi kuzikimbia nyumba zao.