Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu ya kusambaa mionzi ya nyuklia yaongezeka Japan

Hofu ya kusambaa mionzi ya nyuklia yaongezeka Japan

Mionzi ya nyuklia imeanza kusambaa moja kwa moja hewani kufuatia mlipuko katika mitambo ya nyuklia ya Japan iliyoharibiwa na tetemeko na tsunami limesema shirika la kimataifa la nguvu za atomic IAEA.

Moto sasa umezimwa lakini serikali ya Japan imeagiza kuhamishwa kwa watu wanaoishi umbali wa kilometa 20 kutoka kwenye kinu hicho cha nyuklia cha Fukushima Daiichi. Na wale wanaoishi umbali wa kilometa 30 kutoka mtamboni hapo wameagizwa kutotoka nje.

Wakati huohuo shirika la kimataifa la utabiri wa hali ya hewa WMO limeanza kuchunguza ni vipi mionzi kutoka kwenye kinu cha nyuklia cha Japan ilianza kusambaa hewani. Michael Jarraud ni mkuu wa WMO.

(SAUTI YA MICHAEL JARRAUD)

Shirika la WHO linasema kusambaa kwa kiasi kikubwa cha mionzi kuna athari kubwa kwa afya ya jamii, na kuongeza kuwa hatua ya serikali ya Japan kuagiza kuhamishwa kwa watu walio karibu na mtambo wa nyuklia uliolipuka ni mipango inayozingatia usalama wa afya ya jamii kuwaepusha na ajali za nyuklia.