Msaada wa UNICEF wawasili mpakani mwa Tunisia na Libya

Msaada wa UNICEF wawasili mpakani mwa Tunisia na Libya

Tani 47 za msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF umewasili kwenye mji wa Ben Guerdane karibu na mpaka wa Tunisia na Libya.

Msaada huo ni wa mahitaji ya afya, kuwalinda watoto, lishe, maji, na vifaa vya usafi. UNICEF inasema kwa kuwa kuna familia nyingi zinazovuka mpaka zikikimbia machafuko Libya na kuingia Tunisia shirika hilo na washirika wake wanaongeza juhudi za msaada. Jason Nyakundi na taarifa kamili.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

UNICEF pia inajianda kutoa huduma ndani mwa Libya wakati watakaporuhusiwa kuingia nchini humo na pia iwapo hali ya usalama itaruhusu. Kati ya misaada ambayo tayari imewasili kwenye mpaka ni pamoja na vyoo 300 , mablanketi 10,000 , vifaa vya usafi 5,000 na vifaa 100 vya watoto.

Kambi ya Choucha iliyo kwenye mpaka kati ya Tunisia na Libya kwa sasa ni makao kwa takriban familia 300 na watoto 120 wengi wakiwa na umri wa chini ya miaka miwili. Ili kuzuia mkurupuko wowote wa maradhi wizara ya afya kwa ushirikiano na UNICEF na washirika wengine wameanzisha kampeni ya kuchanja watoto dhidi ya maradhi yoyote yanayowaambukiza watoto.

UNICEF pia imeupongeza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wa kutaka kusitishwa kwa ghasia nchini Libya na kuruhusiwa kwa misaada ya kibinadamu kuingia nchini humo.