Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la haki za binadamu limeteua tume kuchunguza Libya

Baraza la haki za binadamu limeteua tume kuchunguza Libya

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeteua tume ya kimataifa ya watu watatu kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Libya.

Tume hiyo itaongozwa na Cherif Bassiouni kutoka Misri ambaye pia ni mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa uhalifu wa kivita, wengine ni Asma Khader, wakili wa masuala ya haki za binadamu kutoka Jordan na Philippe Kirsch kutoka Canada ambaye alikuwa jaji na rais wa kwanza wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu.

Kuteuliwa kwa tume hiyo ni sehemu ya azimio lililopitishwa na baraza la haki za binadamu wakati wa kikao maalumu cha kujadili hali ya Libya. Rais wa baraza la haki za binadamu balozi Sihasak Phuangketkeow amesema sasa kwa kuwa tume imeteuliwa atawasiliana na serikali ya Libya ili kuitaka itoe ushirikiano kusaidia tume hiyo.

Amesema kazi ya tume ni kuchunguza madai yote ya ukiukaji wa haki za binadamu, kupata ukweli uliosababisha hali hiyo na ikiwezekana kuwatambua waliotekeleza na kisha kutathimini hatua za kuwachukulia. Tume hiyo inatarajiwa kuwasailisha ripoti yake kwenye baraza hilo mwezi Juni mwaka huu.