Hali ya Yemen, Bahrain na Saudia inatia hofu:Pillay

Hali ya Yemen, Bahrain na Saudia inatia hofu:Pillay

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema anatiwa hofu na hali inayoendelea nchini Yemen, Bahrain na Saudia.

Amesema kwa Yemen hali ya kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji haijasita na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa mauaji yaliyofanywa na majeshi ya ulinzi na usalama. Raia 37 na maafisa 6 wa usalama wameuawa katika maandamano.

Akizungumzia Bahrain Pillay amesema anahofia usalama wa watetezi watatu wa haki za binadamu , amesema mitandao imekuwa ikitaka wauawe na mingine imekuwa ikiwaita wasaliti. Amesema hofu yake zaidi ni kutokana na maelezo yao binafsi kuwekwa kwenye mtandao na hivyo kutishia usalama wao.

Na kuhusu Saudia Bi Pillay anasema watu ni lazima waruhusiwe kutumia uhuru wao wa kujieleza na kukusanyika bila kuingiliwa na majeshi la usalama. Amezitaka pande zote kujizuia na amelaani matumizi ya nguvu dhidi ya raia Mashariki mwa Saudia.