Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi wanachama wa UM wameombwa kusaidia vikosi vya AMISOM Somalia:Ban

Nchi wanachama wa UM wameombwa kusaidia vikosi vya AMISOM Somalia:Ban

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wametakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuongeza msaada wao kwa wanajeshi 8000 wa muungano wa Afrika (AMISOM) wanaolinda amani nchini Somalia.

Ban ameliambia baraza la usalama kwamba serikali ya mpito ya Somalia na AMISOM wameongeza maeneo wanayoyadhibiti katika mji mkuu Moghadishu baada ya kuwafurusha wanamgambo wa Al-Shabaab.

Ameongeza kuwa serikal na washirika wao wameshika udhibiti wa miji mikubwa ya Kusini mwa Somalia ambayo awali ilikuwa mikononi mwa wanamgambo.

Amesema AMISOM itaweza kutimiza wajibu wake vizuri zaidi kama itapata fedha na vifaa vikiwemo helkopta na msaada wa kijasusi na upelelezi.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Jumuiya ya kimataifa lazima ijitoe zaidi. Kuna mapengo muhimu kwenye msaada wa Umoja wa Mataifa kwa AMISOM na upungufu mkubwa wa vifaa vya kijeshi na fedha. Ninawaomba nchi wanachama kuongeza mchango wao kwenye mfuko wa AMISOM na kulipia vifaa na kulipa nchi zinazochangia wanajeshi.