Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban atoa wito kwa Israel na Lebanon kutekeleza azimio la UM

Ban atoa wito kwa Israel na Lebanon kutekeleza azimio la UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon amesema kuwa kuchelewa kuundwa kwa serikali mpya nchini Lebabon kumezuia kutekelezwa kwa masharti yaliyo kwenye azimio la Umoja wa Mataifa lililomaliza vita kati ya Israel na Hezbollah mwaka 2006.

Serikali ya Lebanon iliyokuwa ikiongozwa na Saad Hariri ilisambaratika kufuatia kujiuzulu kwa mawaziri 11 wa Hezbollah baada ya serikali kukataa kusitisha ushirikiano na mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayochunguza mauaji ya aliyekuwa waziri wa zamani wa Lebanon Rafiq Hariri.

Ban ametoa wito kwa serikali mpya itakayoundwa nchini Lebanon kuendelea kushirikiana na mahakama hiyo iliyoundwa baada ya Umoja wa Mataifa kugundua kuwa uchunguzi uliokuwa ukiendeshwa na serikali ya Lebanon ulikuwa umekumbwa na utata.