Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatima ya Ivory Coast kujulikana Addis Ababa

Hatima ya Ivory Coast kujulikana Addis Ababa

Wakuu wa nchi za Afrika wanakutana mjini Addis Ababa Ethiopia kwenye kikao cha baraza la usalama la umoja wa Afrika katika jaribio la kupata suluhu ya mgogoro wa Ivory Coast.

Viongozi hao wanajadili hatua za kuchukuliwa baada ya juhudi za upatanishi kugonga mwamba mara kadhaa, lakini watajadili kwanza ripoti ya jopo la viongozi watano walioteuliwa na Umoja wa Afrika katika duru ya pili ya upatanishi.

Viongozi hao ni Rais wa Mauritania Mohammed Ould Abdel Aziz, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini, Rais Idris Deby wa Chad na Blaise Compaore wa Burkina Faso.

Na kwa mara ya kwanza Bwana Alassane Ouattara anayetambulika na Umoja wa Mataifa kama mshindi wa uchaguzi wa Urais wa Novemba mwaka jana nchini Ivory Coast anahudhuria mkutano huo wa Addis Ababa. Machafuko yalizuka Ivory Coast baada ya Rais Laurent Gbagbo aliyeshindwa kukataa kuondoka madarakani.