Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay amelaani kushikiliwa waandishi habari Libya

Pillay amelaani kushikiliwa waandishi habari Libya

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay leo amelaani vikali kitendo cha kushikiliwa na uwezekano wa kuteswa kwa waandishi wa habari wa kimataifa wanaojaribu kuarufu kinachoendela nchini Libya.

Waandishi hao walikuwa wakiarifu hali ya Magharibi mwa Libya kwenye mji wa Zawiya. Pillay amesema waandishi habari wana jukumu kubwa la kuarifu ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea na kwa kufanya hivyo wanajikuta katika hatari kubwa. Jason Nyakundi na ripoti kamili.

(RIPOTI YA JAYSON NYAKUNDI)

Waandishi wa habari watatu wa shirika la uingereza la BBC waliripotiwa kupigwa na kudhulumiwa na wanajeshi wa Libya na pia polisi. Pillay amesema kuwa vitendo hivyo dhidi ya waandishi hao wa habari ni ukiukaji wa sheria za kimataiafa.

Amesema kuwa vyombo vya habari ni lazima viruhusiwe kutangaza kinachoendelea nchini Libya bila vizuizi au dhuluma zozote. Pillay amesema kuwa ripoti kuhusu kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya raia kutoka angani na matumizi ya sila nzito kwenye mitaa ya miji zitachunguzwa na kuchukuliwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Ameongeza kuwa huku kukiendelea kubuniwa kwa tume huru ya kimataifa ya kuchunguza yanayoendelea nchini Libya maafisa wa kijeshi ni lazima waelewe kuwa kamwe hawawezi kukwepa mkono wa sheria akisema kuwa kila mmoja aliyehusika atachukuliwa hatua.