Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na IOM yataka msaada zaidi kwa wanaokimbia Libya

UNHCR na IOM yataka msaada zaidi kwa wanaokimbia Libya

Wakihitimisha ziara ya siku mbili nchini Tunisia mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na yule wa shirika la kimataifa la uhamiaji IOM wametoa wito wa kuendelea kwa juhudi za kimataifa kuwasaidia maelfu ya watu wanaokimbia machafuko Libya.

Kamishina mkuu wa UNHCR Antonio Guterres na mkurugenzi mkuu wa IOM William Swing katika taarifa yao ya pamoja wametaja kwamba mpango wa kibinadamu wa kuwasafirisha wakimbizi na wahamiaji umesaidia kupunguza msongamano mipakani mfano katika siku chache maelfu ya Wamisri walikuwa wamerejeshwa nyumbani. Jason Nyakundi na ripoti kamili.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Wawili hao wamesema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kuwa kila mfanyikazi mhamihaji ambaye ameikimbia Libya amefika nyumbani salama na haraka iwezekanavyo. Bwana Swing anasema kuwa wanaoikimbia Libya wamepitia hali ngumu akiongeza kuwa kunahitajika kuongezwa safari za ndege za kuwasafirisha wahamiaji hususan kwenda nchini Bangladesh.

Kwa upande wake bwana Guterres ameipongeza Tunisia kwa kuonyesha kile alichokitaja kama utu kwa kufungua mipaka yake na kutoa makao kwa wahamiaji wanaoikimbia Libya. Wawili hao wameonya kuwa iwapo mapigano yataendelea kuchacha nchini Libya huenda hali ikawa mbaya zaidi. Kwa sasa UNHCR na IOM wanajiandaa kukabiliana na idadi kubwa ya watu wanaokimbia Libya.