Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake milioni 16 wanaishi na virusi vya HIV:UNAIDS

Wanawake milioni 16 wanaishi na virusi vya HIV:UNAIDS

Kati ya watu milioni 34 wanaoishi na virusi vya HIV milioni 16 kati yao ni wanawake na idadi inaongezeka kwa mujibu wa Mariangela Simao mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na ukimwi UNAIDS.

Akizungumza mjini Geneva katika maadhimisho ya miaka 100 ya siku ya kimataifa ya wanawake amesema miaka 30 tangu kuzuka kwa ugonjwa wa ukimwi hakujafanyika juhudi za kutosha kukabili ugonjwa huo miongoni mwa wanawake na wasichana.

Bi Simao amesema UNAIDS na wafadhili wengine wameandaa ajenda ya kushughulikia vyema zaidi mahitaji ya wanawake katika masuala ya ukimwi na virusi vya HIV.

Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wote wenye virusi vya HIV wako Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara na katika eneo hilo wasichana wako mara nne hadi mara nane zaidi katika hatari ya kuambukizwa virusi kuliko wanaume. Amesema HIV bado ni moja ya sababu kubwa ya vifo na maradhi miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuweza kuzaa.