Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki hupuuzwa baada ya machafuko na majanga:Rolnik

Haki hupuuzwa baada ya machafuko na majanga:Rolnik

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za nyumba Raquel Rolnik leo ameonya kwamba viwango vya haki za binadamu na hasa haki za nyumba bora hazijawekwa kwenye sera za hali ya baada ya machafuko au ujenzi mpya baada ya majanga.

Amesema hali ambayo ina athari kubwa kwa wasiojiweza.Bi Rolnik ameyasema hayo mjini Geneva kwenye baraza la haki za binadamu katika ripoti yake ya mwaka . George Njogopa na taarifa zaidi.

( RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Katika ripoti yake hiyo mtaalumu huyo amesisitiza kuwa madhara yatokanayo baada ya kuwepo kwa machafuko yasiishie tu kwa kuangalia athari zinazojitokeza kimaumbele kama vile uharibifu wa mali na watu kuangukia kwenye mtawanyiko, lakini lazima pia kuangalia maeneo mengine ambayo ni muhimu kabisa ikiwemo kuvurugika kwa jamii na mifumo mingine ya maisha.

Ripoti hiyo pia imeangazia suala tete la ardhi ambalo mtaalamu huyo amedai kuwa kutokana na unyeti wake lazima liangaliwe kwa karibu kwani uzoefu unaonyesha kwamba machafuko mengi yanapojitokeza suala la umilikaji wa ardhi linaachwa bila kutafutiwa ufumbuzi wa kuduma.

 

Ametolea mfano kwamba baadhi ya familia ambazo humilika maeneo yaliyoendelezwa vyema lakini machafuko yanapotokea maeneo hayo yanasalia mikononi mwa makundi mengine ya watu jambo ambalo amesisitiza kuwa ni la kuvunja moyo kwa familia zilizoendelea maeneo hayo.