Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko Ivory Coast yatatiza misaada:UNHCR

Machafuko Ivory Coast yatatiza misaada:UNHCR

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanapunguza operesheni zake nchini Ivory Coast wakati hali ya usalama inazidi kuzorota nchini humo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesitisha operesheni zake kwenye eneo la Magharibi mwa nchi hiyo ambako maelfu ya wakimbizi wa ndani ambao ni Waivory Coast walikuwa wanaishi. UNHCR inaonya kwamba nafasi ya misaada ya kibinadamu inatoweka haraka nchini humo.

Mapigano makali yamearifiwa kuzunguka mji wa Magharibi wa Duekoue ambako UNHCR ilikuwa inajenga kambi ya kuwahifadhi wakimbizi wa ndani wapatao 70,000. Melissa Fleming kutoka UNHCR anasema hali ya usalama pia inazidi kuwa mbaya kwenye mji mkuu Abidjan ambako zaidi ya watu 200,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani.

(SAUTI YA MELISA FLEMING)

Zaidi ya watoto milioni moja wanatarajiwa kupata chanjo wiki ijayo dhidi ya surua mjini Abidjan lakini shirika la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la afya duniani WHO wanasema huenda chanjo hiyo ikawa katika hatihati kutokana na usalama mdogo.