Skip to main content

Mahakama ya ICC kuichunguza Libya

Mahakama ya ICC kuichunguza Libya

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC iliyoko The Hague itachunguza madai kwamba serikali ya kiongozi wa Libya Muammar Al-Qadhafi imewakandamiza waliokuwa wakifanya maandamano ya amani.

Mahakama hiyo imesema kwa tathimini ya awali ya taarifa zilizopatikana zinaonyesha kwamb uchunguzi umekubaliwa.  Mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo Luis Moreno Ocampo anatarajiwa kuwasilisha mtazamo wa madai ya makosa yaliyotekelezwa na serikali ya Libya kesho Alhamisi.

Kwa mujibu wa duru za habari zaidi ya watu 1000 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wafuasi wa Rais Qadhafi walipowafyatulia risasi raia waliokuwa wakipfanya kampeni za kumuondoa madarakani.

Kufuatia uchunguzi Bwana Ocampo atawasilisha kesi kwa majaji wa ICC ambao wataamua endapo watoe vibali vya kukamatwa au la. Baraza la usalama liliiomba mahakama ya ICC wiki jana kuchunguza ukatili wanaofanyiwa waandamanaji waliokuwa wakitekeleza haki yao kwa amani.