Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia na makundi ya wachache yanastahili kulindwa nchini Libya:UM

Raia na makundi ya wachache yanastahili kulindwa nchini Libya:UM

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kukomesha ubaguzi wa rangi imeitolea wito jumuiya ya kimataifa na mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa kutafuta hatua za haraka za kuwalinda makundi ya walio wachache nchini Libya .

Kamati hiyo imesema makundi ya wasio raia, wahamiaji, wafanyakazi wahamiaji, wakimbizi na makundi mengine ya walio wachache nchini Libya yako katika hatari katika kipindi hiki kigumu cha machafuko. Alice Kariuki na taarifa kamili.

(RIPOTI YA ALICE KARIUKI)

Katika taarifa iliyotolewa wiki hii katika kutoa onyo la mapema na kutaka hatua zichukuliwe bodi ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa moja kwa moja wa kuchukuliwa hatua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , kwa ushirikiano na vyombo na watu wengine kwenye Umoja wa Mataifa na hasa kamishina mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi, kamishina mkuu wa haki za binadamu na mashirika mengine ya kikanda.

Kamati hiyo ambayo kwa sasa inakutana mjini Geneva inatiwa hofu na mapigano yanayoendelea hivi sasa nchini Libya na athari zake kwa raia wa kigeni na makundi mengine ya walio wachache ambao wanaishi nchini humo .

Kundi la wataalamu binafsi wa Umoja wa Mataifa wamegusia matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia nchini Libya na vitendo vya kikatili dhidi ya raia wa kigeni na pia taarifa la wimbi kubwa la watu wanaokimbia katika nchi jirani.