Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa haraka wa chakula unahitajika Libya:Sheeran

Msaada wa haraka wa chakula unahitajika Libya:Sheeran

Mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP Josette Sheeran aliyezuru mpaka baina ya Libya na Tunisia jana amesema hali ya maelfu wanaokimbia mchafuko ni mbaya na msaada wa haraka unahitajika.

Amesema alichokishuhudia ni bayana kwamba dunia lazima iongeze msaada na kuchukua hatua kuzuia janga la kibinadamu nchini Libya na ametoa wito wa kuwezesha misaada kuwafikia maelfu ya wanaouhitaji hasa Magharibi mwa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa kusitisha msaada wa chakula kusitumiwe kama silaha na kusema matatizo mawili makubwa yanashughulikiwa na WFP hivi sasa nayo ni kutoa msaada wa dharura wa chakula kwa wanaokimbi na kuvuka mpaka kuingia Tunisia na Misri na pili tishio kwa mfumo wa ugawaji chakula hususan Libya ambako ghala limevamiwa na kuvuruga mfumo wa ugawaji.

(SAUTI YA JOSETTE SHEERAN)

Bi Sheeran pia ametoa wito kwa mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na yasio ya kiserikali kusaidia kutoa msaada wa chakula, malazi, na madawa kwa wakati huu na katika siku zijazo nchini Libya. Amesema dola milioni 38.7 zinahitajika kutoa msaada wa chakula kwa watu milioni 2.7 Libya, Misri na Tunisia.