Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lamuwekea vikwazo Qadhafi na kuitaka ICC kuichunguza Libya

Baraza la usalama lamuwekea vikwazo Qadhafi na kuitaka ICC kuichunguza Libya

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kumuwekea vikwazo kiongozi wa Libya Muammar Qadhafi na kuitaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kuchunguza uwezekano wa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Wajumbe 15 wa baraza hilo walipiga kura ya bila kupingwa kupitisha azimio ambalo litazuia samani zote za Qadhafi pamoja na za familia na wasaidizi wake wa ngazi ya juu. Pi aimemuwekea vikwazo vya usafiri.

Vikwazo hivyo ni pamoja na vya silaha na hatua za kusitisha matumizi ya askari mamluki wanaoaminika kuwepo na kushiriki katika machafuko Libya.

Pia azimio hilo limeitaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu kuchunguza vitendo vya Libya kuwasaka na kuwaadhibu waandamanaji wanaoipinga serikali ,jambo ambalo ni uwezekano wa uhalifu dhidi ya ubindamu. Hatua hiyo ni nadra sana kuchukuliwa na baraza la usalama.

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Susan Rice, ameliambia baraza hilo baada ya upigaji kura kwamba azimio hilo ni ujumbe mzito kwa Qadhafi.

(SAUTI YA SUSAN RICE)

Wakati kiongozi anang'ang'ania kusalia madarakani na kutumia ghasia dhidi ya watu wake basi amepoteza mwelekeo na haki ya kutawala na anahitajika kuchukua hatua muafaka kwa ajili ya taifa lake kwa kuondoka sasa.

Azimio namba 1970 limepitishwa katika kikao maalumu cha baraza la usalama kilicchofanyika Jumamosi usiku.