Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amesikitishwa na matumizi ya watoto kujitoa muhanga Pakistan

Ban amesikitishwa na matumizi ya watoto kujitoa muhanga Pakistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesikitishwa na ripoti kwamba mtoto ametumiwa kufanya shambulio la leo la kujitoa muhanga kwenye kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Mardan Kaskazini Magharibi mwa Pakistan.

Shambulio hilo limesababisha vifo vya watu wengi na kujeruhi wengine. Kwa mujibu wa duru za habari mvulana aliyefanya shambulio hilo alikuwa amevalia sare za shule, na aliingia kwenye kambi hiyo ya jeshi na kujilipua, akafa yeye na watu wengine 27, wakiwemo makuruta wengi.

Katibu Mkuu amelaani vikali shambulio hilo na hasa kuwatumia watoto kutekeleza vitendo hivyo vya kigaidi. Ban pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kwa serikali ya Pakistan.