Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe maalumu wa UNESCO kuzuru Cambodia na Thailand

Ujumbe maalumu wa UNESCO kuzuru Cambodia na Thailand

Ujumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa umetumwa kwenda Cambodia na Thailand ili kusaidia kutatua mzozo dhidi ya hekalu la Preah Vihear.

Hekalu hilo la Wahindu lililojengwa karne ya 11 liliingizwa katika orodha ya urithi wa dunia mwaka 2008.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO Irina Bokova amesema maeneo ya kitamaduni ambayo ni urithi wa dunia asilani hayatakiwi kuwa chanzo cha mizozo. Bi Bokova anamtuma mjumbe maalumu kwenda Bangkok na Phnom Penh ili kujadiliana na pande zote katika mvutano huo.

Hekalu la Preah Vihear ni mali ya Cambodia kwa mujibu wa uamuzi wa makahakama ya kimataifa mwaka 1962, lakini lango lake kuu la kuingilia liko upande wa Thailand na nchi zote zinadai kuwa wamiliki halali wa sehemu inayozunguka hekalu hilo. Mapigano yamezuka karibuni kati ya nchi hizo mbili wakigombea masuala ya mipaka.