Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za haraka zinahitajika kutatua mzozo wa Ivory Coast:UNHCR

Hatua za haraka zinahitajika kutatua mzozo wa Ivory Coast:UNHCR

Mvutano wa kisiasa nchini Ivory Coast hadi leo umewatawanya watu zaidi ya 70,000 limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kwa mujibu wa shirika hilo nusu ya watu hao wamekimbilia nchi jirani ya Liberia huku wengine 35,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani Magharibi mwa Ivory Coast. Kamishina mkuu wa UNHCR Antonio Guterres amesema kutomalizika kwa mtafaruku huo wa kisiasa kunazidi kuathiri hali ya kibindamu katika nchi hiyo. Amesema suluhisho la haraka la muda mrefu linahitajika na ikishindikana basi kuna hatari kubwa kwa mamilioni ya watu wan chi hiyo ambao watalazimika kufunga virago.

UNHCR inasema ongezeko la wakimbizi wa Ivory Coast wanaotafuta usalama katika nchi za jirani litaleta athari kwenye eneo hilo na hasa Liberia ambayo bado inajijenga upya baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Guterres amesema ukizingatia hali halisi naipongeza Liberia kwa sera ya kufungua mipaka yake na watu wa Liberia ambao wamefungua mioyo na nyumba zao kuwapokea wakimbizi na kushiriki nao vichache walivyonavyo. Hatua ya kisiasa ya haraka ya kimataifa inahitajika kumaliza mzozo huo na kurejesha utulivu. Watu wa Ivory Coast wanapaswa kuwa salama nyumbani kwao na sio kulazimika kukimbia kuweza kupata usalama.