Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi ya aliyekuwa Rais wa Liberia inaelekea ukingoni The Hague

Kesi ya aliyekuwa Rais wa Liberia inaelekea ukingoni The Hague

Wakili wa aliyekuwa Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor amearifiwa kuondoka mahakamani The Hague kwa hasira wakati kesi ya mtuhumiwa huyo iliyo katika hatua za mwisho ikiendelea.

Wakili huyo Courtenay Griffiths aliyekuwa akijaribu kuwasilisha maelezo ya mwisho ya kesi baada ya siku 20 wa muda wa kuwasilisha ombi kupita alipandwa na jazba baada ya majaji wa mahakama kukataa ombi lake.

Bwana Taylor anakabiliwa na makosa 11 likiwemo la kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1990 na kuwasaidia waasi ambayo ni uhalifu wa kivita na ukatili dhidi ya ubinadamu. Taylor amekana mashitaka yote yanayomkabili.

Waendesha mashitaka watakamilisha kuwasilisha maelezo yao leo Jumanne huku upande wa utetezi utafanya hivyo kesho Jumatano huku hitimisho likiwa siku ya Ijumaa. Hukumu inatarajiwa katikati ya mwaka huu wa 2011 na endapo Bwana Taylor atakutwa na hatia basi atatumikia kifungo nchini Uingereza.