Skip to main content

Mafuriko Sri Lanka yameleta athari kubwa:OCHA

Mafuriko Sri Lanka yameleta athari kubwa:OCHA

Nchini Sri Lanka, mvua kubwa zilizonyesha katika siku saba zilizopita zimesababisha mafuriko katika wilaya 18 zikiwemo za Mashariki, Kaskazini, Katikati, Uva na majimbo ya Kusini .

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA mito mingi imefurika, barabara nyingi hazipitiki kwa kujaa maji, na kutoa changamoto kubwa kwa shughuli za misaada zinazoongozwa na serikali .

Uharibifu mkubwa katika nyumba na mashamba umeongezeka. OCHA inasema idadi ya waathirika na wasio na makazi inaendelea kuongezeka na msaada kwa sasa unajikita kutoa maji safi , vitu visivyo chakula, malazi na chakula.

Kituo kinachohusika na udhibiti wa majanga DMC kinasema hadi kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita watu 984,256 wameathirika na jumla ya watu 185,820 sawa na familia 50,121 hawana makazi na kuhifadhiwa kwenye makambi ya muda 543 katika wilaya 13.

Serikali inaoongoza harakati za misaada ikiungwa mkono nad WFP, UNICEF, UNHCR, IOM na mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGOs. WFP, OCHA na UNDP wamepeleka wafanyakazi zaidi katika maeneo yaliyoathirika.