Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afghanistan yatia saini makubaliano kutoingiza watoto jeshini

Afghanistan yatia saini makubaliano kutoingiza watoto jeshini

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu katikia masuala ya watoto kwenye migogoro

Radhika Coomaraswamy amerejea kutoka ziara ya siku tatu nchini Afghanistan ambako ameshuhudia makubaliano yakitiwa saini kati ya serikali ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa kusitisha uingizaji wa watoto jeshini na ukiukaji mwingine kwa majeshi yote ya nchi hiyo.

Mwakilishi huyo Radhika Coomaraswamy pia amekutana na jenerali Petraeus kamanda wa majeshi ya kimataifa ya msaada ISAF na yule wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan, viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo na viongozi wa kidini.

Kutiwa saini makubaliano hayo ya kuchukua hatua kumetokana na orodha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Matraifa iliyoko kwenye ripoti ya mwaka 2010 kwenye baraza la usalama ambayo imelitaja jeshi la polisi la nchi hiyo kuwafunza na kuwatumia watoto.

Bi Coomaraswamy amesema kwa kutia saini na kutekeleza makubaliano hayo jeshi la polisi la Afghaniastan litaweza kuondolewa kwenye orodha hiyo baada ya kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa kwamba sera na taratibu zimefuatwa na kutekelezwa kikamilifu kuzuia uingizaji wa watoto jeshini na kwamba ukiukaji wowote umechunguzwa kwa kina na wahusika kuwajibishwa.

Makubaliano hayo yametiwa saini na waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan Zalmai Rassoul na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNAMA) Staffan de Mistura mjini Kabul.

Coomaraswamy amesema hii ni hatua muhimu katika kuelekea kuwalinda watoto nchini Afghanistan lakini cha muhimu zaidi ni utekelezaji wa makubaliano hayo kuendelea na majibu ndioyo yatakayothibitisha mpango huo haujaishia tuu kwenye karatasi na kuwekwa kwenye makabati.

Makubaliano hayo yaanza kutekelezwa mara moja kwa kuwa na hatua madhubuti, kwa wakati maalumu na shughuli zitakazokuwa zikifanywa na wizara mbalimbali za Afghanisatan kwa msaada wa mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF.