Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matatizo ya ukame Kenya yapatiwe suluhu:Amos

Matatizo ya ukame Kenya yapatiwe suluhu:Amos

Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa akiwa mjini Nairobi hii leo amesema changamoto nyingi za kibinadamu zinazoikabili Kenya nyingi zikitokana na kujirudia kwa hali ya ukame na ukuaji wa haraka wa miji zinaweza kushughulikiwa kwa kutumia njia zitakazozihakikishia jamii uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema kuendelea na juhudi za kupunguza athari za ukame kutahakikisha kurejea katika maisha ya kawaida na kuwasaidia watu kukabili tatizo la ukame ikirejea tena. Mkuu huyo Valarie Amos yuko katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu nchini Kenya na Somalia.

Amesema upungufu wa chakula na maji uliosababishwa na uhaba wa mvua unaweza kuepukwa endapo ardhi yenye rutba ya Kenya itatumika kwa kilimo cha umwagiliaji , kuwapa maji wafugaji, kuimarisha ufugaji kwa kudhibiti magonjwa na wanyama bora, na kufanya masoko ya mifugo kuwa yanayoaminika.

Bi Amos amesema kujirudia kwa hali ya ukame kunasababisha jamii kuhamia maeneo ya mijini ambayo yanaukosefu wa nyenzo za kumudu ongezeko la watu na hivyo kuwafanya watu hao kuishi kwenye mitaa ya mabada ambako kuna mrundikano wa watu, hakuna huduma muhimu za afya, malazi duni, maji haba na mazingira machafu.

Akiwa Kenya pia Bi amos amekutana na maafisa wa ngazi za juu wa serikali , maafisa wa Umoja wa Mataifa, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa jumuiya za kijamii.