Wenye matatizo ya mafuta mengi mwilini hawapati tiba:WHO

Wenye matatizo ya mafuta mengi mwilini hawapati tiba:WHO

Utafiti mkubwa kabisa wa afya kuwahi kufanyika na kuhusisha watu milioni 147 duniani umeonyesha kwamba watu wengi wenye kiwango kikubwa cha mafuta mwilini hawapati tiba inayohitajika kuwapunguzia hatari ya maradhi ya moyo kama mshituko na kiharusi.

Matatizo ya moyo ni miongoni mwa magonjwa yanayoua watu wengi, ambapo milioni 17 hufa kila mwaka duniani kote. Utafiti huo uliochapishwa leo na shirika la afya duniani WHO unasema watu wengi walio katika hatari wanaishi Uingereza, Ujerumani, Japan, Jordan, Mexico, Scotland, Thailand na Marekani na hawajui kwamba wanahitaji matibabu ambayo ni dawa za gharama nafuu.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la WHO ni wa kwanza kuonyesha kiwango cha mapungufu ya tiba kwa walio na matatizo ya mafuta mengi mwilini. Thailand asilimia 78 ya watu wazima waliohojiwa hawajawahi kupimwa, wakati Japan asilimia 53 ya watu wazima walichunguzwa afya zao lakini hawajatibiwa.