Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa haki za binadamu ameutaka uongozi wa Misri kusikiliza wito wa demokrasia na kufanya mabadiliko

Mkuu wa haki za binadamu ameutaka uongozi wa Misri kusikiliza wito wa demokrasia na kufanya mabadiliko

Waandamanaji nchini Misri wamepongezwa na Umoja wa Mataifa kwa ujarisi na maandamano ya amani.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi Navi Pillay hata hivyo amesema anashitushwa na ongezeko la haraka la idadi ya wanaokufa, huku ripoti zisizo rasmi zinasema waliokufa hadi sasa ni 300 na wengine 3000 wamekamatwa.

Mkuu huyo wa haki za binadamu amesema kwa kuandamana watu wa Misri wanaonekana kuukataa mfumo ambao umewanyima haki zao za msingi na kutekeleza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo utesaji. Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya kamishina mkuu wa haki za binadamu.

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

Kamishina mkuu amekaribisha tangazo la jeshi la kutotumia nguvu dhidi ya watu, lakini anahofia hali ya kutokuwepo usalama iliyosababishwa na kujiondoa mitaani kwa polisi . Amesema kufanya hivyo ni ukiukaji wa haki ya usalama na ulinzi wa watu, na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kwanini serikali imechukua uamuzi wa kuuweka umma katika hatari ya namna hiyo.