Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa UM ameanza ziara Kenya na Somalia:OCHA

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa UM ameanza ziara Kenya na Somalia:OCHA

Mratibu wa shirika la umoja wa mataifa la masuala ya kibinadamu OCHA Valerie Amos anaanza ziara yake ya kwanza Afrika ya Mashariki kesho tarehe mosi February ambapo atazuru Kenya na Somalia.

Katika ziara hiyo ya siku tatu Bi Amos atatathimini hali ya ukame katika mataifa hayo mawili. Akiwa Kenya atakutana na viongozi wa serikali na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa wa kibidamu ikiwa ni pamoja na kuwahifadhi wakimbizi kwa miongo miwili sasa. Atakutana pia na washirika wengine wa maendeleo na misaada ikiwemo mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, jumuiya za kijamii na jumuiya za wahisani. Kikubwa watakachozungumza ni mikakati imara ya kuchagiza hatua za mapema za kukabiliana na hali inayojirudia rudia ya ukame.

Kutoka Kenya Bi amos ataelekea Somalia ambako atatembelea makazi ya wakimbizi wa ndani, na kukutana na serikali, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali.