Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 31,000 wa Ivory Coast wameingia Liberia:UNHCR

Wakimbizi 31,000 wa Ivory Coast wameingia Liberia:UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema idadi ya wakimbizi wa Ivory Coast wanaoingia Liberia inaongezeka kila siku.

Shirika hilo linasema  tangu mapema mwezi wa Disemba zaidi ya wakimbizi 30,000 wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake wamemiminika nchini humo wakijitafutia hifadhi katika maeneo ya maporini na vijijini. Wakimbizi hao hata hivyo wanaendelea kuishi kwenye mazingira magumu na ya hatarini kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji salama ya kuchwa.

Kwa mfano katika kijiji kimoja uhaba wa maji umeanza kujitokeza hasa baada ya kuwepo kwa ongezeko la mahitaji ambayo kumefanya kuharibika kwa mabomba kadhaa yaliyokuwa yakisuma maji, na kuna wasiwasi kwamba mabomba machache yaliyosalia huenda nayo yakazidiwa.

Mama mmoja amesema kuwa kutokana na uhaba huo wa maji kumewazimu kukusanya maji kwenye visima visivyo rasmi na mifereji michafu jambo ambalo limeanza kuhatarisha afya zao kwani baadhi ya watoto wameanza kupata magonjwa ya kuambukizwa.

Pia kuna hali ya kukwama kwa huduma nyingine za kijamii ikiwemo uhaba wa madarasa kwa wanafunzi wa elimu ya msingi kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Ivory Cost wanaendelea kumiminika.Serikali ya Liberia kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF imekuwa ikifanya juu chini kukabiliana na hali hiyo.