Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathirika wa mafuriko Pakistan wajenga upya maisha:IOM

Waathirika wa mafuriko Pakistan wajenga upya maisha:IOM

Wakati huohuo miezi sita baada ya mafuriko kuikumba Pakistan idadi kubwa ya waliopoteza nyumba zao na tegemeo lao la kimaisha wamerejea kwenye miji na vijijini vyao wakijaribu kujenga upya nyumba zao.

Mamia ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwa usaidizi wa jamii ya kimataifa yako kwenye mstari wa mbele tayari kusaidia lakiki hata hivyo yanakabiliwa na uhaba wa fedha. Mafuriko hayo yaliyoikumba Pakistan mwaka uliopita yaliharibu takriban nyumba milioni 1.7 na kuwaacha karibu watu milioni 11 bila makao. George Njogopa anaripoti

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Hatua kwa hatua hali ya maisha kwa wananchi wa Pakistan ambao waliathiriwa vibaya na mafuriko sasa yanaanza kurejea kwenye hali ya kawaida,lakini hata hivyo safari bado ni ndefu. Mafuriko hayo yaliyoibiga nchi hiyo mwaka uliopita wa 2010 ambapo sasa imetimia miezi sita yaliharibu zaidi ya nyumba milioni 1.7 na kufanya watu milioni 11 kukosa makazi.

Katika jimbo la Punjab pekee madhara yaliyosababishwa na mafuriko hayo yanatajwa kuwa mara dufu yakifananishwa na tetemeko la ardhi lililoikumba Haiti mwaka uliopita. Nyumba nyingine ziliharibiwa vibaya katika jimbo la Dadu lililoko Kusin mwa Sindh ambako madhara yake yanapindukia yale yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi la mwaka 2004 katika eneo la Aceh.Tayari jumuiya za kimataifa zimeisaidia nchi hiyo kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1.1 kwa ajili ya kuikarabati upya.

Katika makadirio yake ya awali Umoja wa Mataifa ulisema unahitaji kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1.96 ili kuyafikia maeneo yote yaliyoharibiwa. Katika maeneo mbalimbali wananchi wakishirikiana na taasisi za kimataifa wamekuwa wakiendesha miradi na ujenzi wa miundo mbinu ili kuijenga upya nchi hiyo.