Mamilioni kupoteza uwezekano wa kupata dawa za kurefusha maisha: UM

Mamilioni kupoteza uwezekano wa kupata dawa za kurefusha maisha: UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu haki ya afya Anand Grover ameonya kwamba mswada wa makubaliano ya biashara huru baina ya muungano wa Ulaya na India (FTA) huenda ukawazuia watu kote duniani kupata fursa ya dawa za kuokoa na kurefusha maisha.

Amesema mamilioni ya watu katika nchi zinazoendelea wanategemea madawa hayo kutoka India kwa gharama nafuu hivyo udhibiti wa utengenezaji wa madawa hayo utakuwa na athari kubwa katika afya ya jamii na kuathiri haki ya afya kwa mamilioni ya watu.

Uwezo wa India kuzalisha madawa hayo na kuyauza kwa gharama nafuu kunatokana na sheria zake za umiliki wa kitaaluma, hasa katika masuala yanayohusiana na sheria za biashara ambazo zinairuhusu nchi hiyo kuzalisha daawa salama na za manufaa makubwa.

Lakini kwa mujibu wa Bwana Anand baadhi ya vipengee katika makubaliano ya FTA ambayo kwa sasa yako katika mjadala baina ya India na muungano wa Ulaya vinatishia mfumo mzima wa uzalishaji.