Ban alaani shambulio la bomu uwanja wa ndege Moscow

Ban alaani shambulio la bomu uwanja wa ndege Moscow

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio la bomu lililofanyika leo kwenye uwanja wandege wa Domodedovo mjini Moscow Urusi ambalo limekatili maisha ya wengi na kujeruhi wengine.

Katika taarifa iliyosomwa kupitia msemaji wake, Ban amesema amesikitishwa na tukio hilo ambalo amesema ni la kulaaniwa na halina msingi dhidi ya watu wasio na hatia. Ban ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kuonyesha mshikamano wake kwa watu na serikali ya shirikisho ya Urusi.

Kwa mujibu wa duru za habari serikali ya Urusi imesema shambulio hilo la bomu huenda limetekelezwa na mtu wa kujitoa muhanga na serikali imeongeza ulinzi katika viwanja vya ndege vya Moscow na mifumo mingine ya usafiri.