Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID yaiamarisha ulinzi kwenye kambi Darfur

UNAMID yaiamarisha ulinzi kwenye kambi Darfur

Vikosi vya kimataifa vya kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan vimelazimika kuimarisha hali ya ufuatiliaji kwenye maeneo ya kambi ambako kunahifadhiwa wakimbizi wa ndani kufutia operesheni ya ghafla iliyofanywa hapo jumapili na vikosi vya serikali ambavyo havikufanya mawasiliano yoyote na vikosi hivyo vya kimataifa.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na vikosi hivyo vya kimataifa UNMID, msako huo uliofanywa kwenye kambi ya Zam Zam iliyopo pembezoni mwa eneo lijulikanalo El Fasher,ulilenga kuwakamata makundi ya kihalifu,pamoja na kusambaratisha silaha na bidhaa haramu.

Katika msako huo, serikali imesema kuwa ilifanikiwa kuwatia mbaroni watu 37, magari 10, pamoja na silaha kadhaa za moto. Hata hivyo UNMID imesema kuwa kitendo hicho kilichofanywa na vikosi vya serikali kinakiuka makubalino ya mkataba baina ya vikosi hivyo vya kimataifa na serikali hiyo.Serikali kabla ya kuchukua hatua hiyo ilipaswa kutoa taarifa ya mapema kwa UNAMID.