Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2010 ndio uliokumbwa na majanga hatari zaidi ya kiasili:UM

Mwaka 2010 ndio uliokumbwa na majanga hatari zaidi ya kiasili:UM

Kulingana na tamwimu za Umoja wa Mataifa ni kuwa karibu watu 300,000 waliuawa na majanga ya kiasili mwaka 2010 wakati baadhi ya majanga mabaya zaidi yakiwa ni pamoja na tetemeko la ardhi lililotokea nchini Haiti na kusababisha vifo vya watu zaidi ya watu 222,000 na joto nchini Urusi pamoja na moto wa msituni vilivyosababisha vifo vya watu 56,000.

Idara ya Umoja wa Mataifa inayopambana na majanga inasema kuwa mwaka 2010 ulikumbwa na majanga hatari zaidi ya kiasili kwa muda wa miaka 20 iliyopita. Hata hivyo majanga ya kiasili 373 yalishuhudiwa na kuwaathiri karibu watu milioni 210 na pia kusababisha uharibifu unaokadiriwa kuwa wa dola bilioni 110. Margareta Wahlström mwakilishi wa idara ya Umoja wa Mataifa inayopambana na majanga anasema kuwa ikiwa mataifa hayatachukua hatua za mapema hasara inayosababisha na majanga kama hayo itaendelea kuongezeka

(SAUTI YA MARGARETA WAHLSTROM)

Mafuriko yaliongoza kwa idadiaya majanga yaliyotokea mwaka 2010 kwa visa 182 , yakifuatiwa na majanga ya vimbunga , hali mbaya ya hewa na mitetemeko ya ardhi mtawalia.