Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama Somalia utategemea mikakati ya kisiasa:Mahiga

Usalama Somalia utategemea mikakati ya kisiasa:Mahiga

Naibu waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia na waziri wa mipango na ushirikiano wa kimataifa Abdweli Mohamed Ali pamoja na mwakilishi maalumu wa mwenyekiti wa muungano wa Afrika na mkuu wa vikosi vya kulinda amani Somalia AMISOM Bourbacar G. Diarra na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia dr Augustine Mahiga leo wameanza mkutano wa kamati ya usalama nchini Djibouti.

Akihutubia mkutano huo naibu waziri mkuu wa Somalia ameelezea umuhimu wa kamati hiyo katika kutimiza moja ya malengo muhimu la kurejesha amani na usalama Somalia. Kwa upande wake dr Mahiga amesisitiza kwamba mikakati ya usalama kwa Somalia lazima itokane na malengo ya kisiasa hususani katika kipindi kifupi kilichosalia cha serikali ya mpito.

Mahiga amesema mikakati ya usalama inaambatana na nia ya serikali kutekeleza malengo muhimu ya kisiasa ya kupanua wigo wake, upatanishi na kusaidia majadiliano ya mchakato wa uundwaji wa katiba mpya.

Akiishukuru jumuiya ya kimataifa kwa msaada wao Mahiga amesema mfuko kwa ajili ya Somalia uliotengwa kuwalipa walinda amani wa AMIS na kushughulikia mahitaji ya wanajeshi wa serikali ya mpito unahitaji msaada wa haraka.