Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya mavuno Niger bado ina utapia mlo : WFP/FAO

Licha ya mavuno Niger bado ina utapia mlo : WFP/FAO

Niger imeongeza karibu mara mbili ya uzalishaji wa chakula mwaka mmoja uliopita na kuwatoa mamilioni katika hatari ya baa la njaa kwa mujibu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.

Msimu mzuri wa mvua kwa mwaka 2010 ukichanganya na ugawaji wa mbegu bora zaidi ya tani 3400 vimesaidia uzalishaji wa nafaka na kufikia tani milioni 5.6 kiwango ambacho ni asilimia 60 zaidi ya mwaka 2009. Tathimini iliyofanywa na FAO na WFP inasema Niger sasa na akiba kubwa ya nafaka ambayo itatumika kujazia akiba iliyotumika wakati wa ukame.

Richard Verbeek ni mwakilishi wa WFP nchini Niger, anasema licha ya uzalishaji mkubwa kiwango cha utapia mlo bado kikubwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na hatua muhimu kuboresha uwekezaji wa lishe zitahitajika ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.

(SAUTI YA RICHARD VERBEEK)

Ameongeza kuwa mwaka 2010 serikali ya Niger ikisaidiwa na Umoja wa Mataifa ilizindua mpango mkubwa wa msaada wa kibinadamu ambao ulikabiliana na tatizo la chakula ambalo liliwaweka watu zaidi ya milioni saba katika hatari ya baa la njaa.