Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeomba dola milioni 87 kuwasaidia wakimbizi wa Ivory Coast

UM umeomba dola milioni 87 kuwasaidia wakimbizi wa Ivory Coast

Umoja wa Mataifa umeomba zaidi ya dola milioni 87 kusaidia operesheni za kibinadamu zitokanazo na mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Ivory Coast.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA imesema dola milioni 55 zitatumika kutoa msaada wa malazi kwa wakimbizi wa Ivory Coast walioko nchini Liberia wakati dola milioni 32 zitasaidia operesheni za misaada nchini Ivory Coast na mataifa manne ya jirani.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba Waivory Coast wapatao milioni mbili wataathirika na mvutano wa kisiasa unaoendelea na kusababisha maaafa ya kibinadamu. Elizabeth Byrs ni msemaji wa OCHA.

(SAUTI YA ELIZABETH BYRS)

Hadi leo Waivory Coast 30,000 wamevuka mpaka na kuingia Liberia, huku wengine 18,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani na kwenda kupata hifadhi kenye maeneo yenye usalama ndani ya Ivory Coast.

Wakati huohuo hofu inaongezeka nchini Ivory Coast na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNOCI walilazimika kufyatua risasi hewani kuwatawanya kundi wa wafuasi wa Laurent Gbagbo. Waziri mkuu wa Kenya Rais Odinga anayewakilisha muungano wa Afrika katika kupata suluhu ya mzozo huo anaendelea na kuwashawishi uwezekano wa kuwepo majadiliano ya ana kwa ana baina ya Gbagbo na Alassane Ouatarra. Nao wakuu wa majeshi wa kutoka baadhi ya nchi za Afrika ya Magharibi wanakutana kujadili hatua za kijeshi zitakazochukuliwa endapo itahitajika.