Utawala wa sheria urejeshwe mara moja Tunisia:Ban

Utawala wa sheria urejeshwe mara moja Tunisia:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ameelezea hofu yake juu ya kuendelea kwa machafuko yanayosababisha kupotea kwa maisha ya watu nchini Tunisia,na ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo kwa pande zote ili kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani n kurejesha utulivu nchini humo.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Ninaitolea wito serikali na washika dau wote husika kuhakikisha wanarejesha utawala wa sheria, wanaheshimu na kukumbatia matakwa ya watu. Tunisia ni lazima irejee kwenye utulivu haraka iwezekanavyo kuhakikisha inafuata njia ya maendeleo.

Ban ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa habari nchini abu Dhabi anakohudhuria kongamano la kimataifa kuhusu nishati. Nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini imeghubikwa na maandamano mitaani katika wiki za karibuni na wananchi waliokasirishwa na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu, ukosefu wa fursa za ajira, ufisadi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uhuru.

Rais wan chi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali, amekimbia nchi wiki iliyopita baada ya maandamano hayo kuchacha na kuzuka kwa ghasia kubwa.