Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakaribisha maafikiano ya ufuatiliaji silaha nchini Nepal

UM wakaribisha maafikiano ya ufuatiliaji silaha nchini Nepal

Mjumbe maalumu ya Umoja wa Mataifa nchini Nepal anayemaliza muda wake, Karin Landgren amekaribisha makubaliano yaliyofikiwa baina ya serikali na chama cha Unified Communist Party of Nepal ya kuwepo kwa ufuatiliaji wa karibu wa silaha.

Pande hizo zimeafikiana kuwepo kwa mfumo maalumu ambao utadhibiti na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa matumizi ya silaha nchini humo makubaliano ambayo yanatizamwa kama nuru njema inayokusudia kuimarisha hali ya usalama na kuwepo kwa hali ya utulivu.

Akizungumzia hatua hiyo, mwakilisho huyo wa Umoja wa Mataifa amepongeza hali hiyo akisema kuwa inaleta faraja na matumaini mapya kwa wananchi wa Nepal kuhusu uimarishwaji wa hali ya ulinzi na usalama.

Mpango huo umekuja kukamilika wakati ambapo ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo uliokuwa na kazi ya kuratibu shughuli za ufuatiliaji wa silaha ukimaliza kazi zake rasmi jana usiku.