Katibu Mkuu wa UM akaribisha kumalizika kwa upigaji kura ya maoni Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa UM akaribisha kumalizika kwa upigaji kura ya maoni Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon leo amekaribisha kumalizika kwa upigaji kura ya maoni ya kuamua hatma ya Sudan Kusini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon Ban pia amewapongeza watu wa nchi hiyo kwa uvumilivu, utulivu na amani waliyoionyesha wakati wa wiki nzima ya upigaji kura. Bwana Ban amepongeza kazi iliyofanywa na tume ya Sudan Kusini ya kusimamia kura hiyo ya maoni (SSRC) mjini Khartoum na ofisi yake ya Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini , na kazi ya vyama vyote viwili kwa kuzingatia vipengee vya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ya (CPA) ambayo yalimaliza vita vya zaidi ya muongo katika ya Sudan kusini na Kaskazini.

Katibu Mkuu amewashukuru nchi wahisani kwa mchango wao wa kusaidia kufanikisha mchakato mzima wa kura hiyo ya maoni, na makundi yote ya waangalizi waliosafiri katika nchi nzima na nchi za nje ili kusimamia na kuangalia zoezi zima.

 Ban amewataka watu na taasisi za Sudan Kusini kuwa wavumilivu na kusubiri hadi tume ya kura ya maoni itakapotangaza matokeo rasmi ya kura hiyo. Matokeo ya kura hiyo ya amaoni iliyoanza Januari 9 na kukamilika leo Januari 15 itaamua endapo Sudan Kusini ijitenge na kuwa taifa huru au isalie katika muungano na Kaskazini.

Kwa mujibu wa tume ya kura ya maoni SSRC matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa Februri pili na itategemea endapo kutakuwa na rufaa zitakazowasilishwa mahakamani au la, hivyo matokeo ya endapo Sudan Kusini itakuwa mjumbe wa 193 wa Umoja wa Mataifa yatatangazwa tarehe 7 au 14 Februari.