Skip to main content

UM unasaidia waathirika wa ukame nchini Kenya

UM unasaidia waathirika wa ukame nchini Kenya

Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaisaidia serikali ya Kenya kukabiliana na upungufu wa chakula na maji uliyoyakumba maeneo mengi ya nchi hiyo kutokana na ukame wa muda mrefu hasa kwenye maeneo makavu yanayokaliwa na wafugaji wa kuhamahama.

Msaada katika jamii zilizoathrika maeneo ya Kaskazini, Mashariki, Kaskazini Mashariki na maeneo ya Pwani ya Kenya ni pamoja na maji, chakula na lishe mbadala kwa watoto imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kibinadamu OCHA. Watu watano wamearifiwa kufariki dunia hadi sasa.

Ukame huo unatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa kilimo na ufugaji na kuleta tafrani kwa maisha ya watu takribani milioni tatu. Bei za chakula zimepanda huku familia nyingi ambazo hazina hazina kipato cha kutosha zikiathirika zaidi.

Serikali ya Kenya na mashirika ya misaada ya kibinadamu watafanya tathimini ya siku 12 kuanzia Jumatatu ijayo kubaini ukubwa wa tatizo imesema OCHA.