Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awaonya wanaoshambulia walinda amani wa UM nchini Ivory Coast

Ban awaonya wanaoshambulia walinda amani wa UM nchini Ivory Coast

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ameyaonya majeshi yanayomuunga mkono anayeondoka madarakani nchini Ivory Coast ambaye amegoma kuachia ngazi licha ya kushindwa uchaguzi, kwamba watawajibika kwa uhalifu wao wa kuvishambulia vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini humo UNOCI.

Katika taarifa iliyosomwa na msemaji wake Ban ameelezea hofu kwamba wanajeshi rasmi na wasio rasmi wanaomuunga mkono Bwana Gbagbo wameanza kushambulia na kuchoma moto magari yanayomilikiwa na UNOCI mpango ambao umekuwa ukisaidia nchini humo kwa miaka saba sasa kuiunganisha tena Ivory Coast baada ya vita vya wenyewe kwa wenye vilivyoigawa mapande mawili nchi hiyo mwaka 2002.

Ban amesema kuanzia asubuhi ya leo kumekuwa na matukio sita ya mashambulizi mjini Abijan ambapo magari ya UNOCI yamechomwa moto. Daktari na dereva wa gari la kubeba wagonjwa walikuwa ni walengwa katika moja ya shambulio na wamejeruhiwa. Pia magari mengine mawili yamechomwa na mengine matatu kuharibiwa.