Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyikazi wa WFP watekwa nyara Darfur Sudan

Wafanyikazi wa WFP watekwa nyara Darfur Sudan

Wafanyakazi watatu wa ndege wanaofanya kazi na mpango wa Umoja wa Mataifa wa chakula duniani WFP wametekwa nyara kwenye jimbo la Darfur Sudan.

Kwa mujibu wa duru za habari zikimnukuu msemaji wa mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika Darfur UNAMID Chris Cycmanick watu hao walitekwa usiku wa Jumatano Januari 12 kilometa 75 Kusini Mashariki mwa mji wa Geneina ambao ni mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi.

Wafanyakazi hao ni raia wa Bulgaria. Shirika la WFP limesema wafanyakazi hao walitekwa na watu wenye silaha kwenye uwanja mdogo wa ndege. Serikali ya Bulgaria imethibitisha kwamba raia wake hao watatu waliokuwa marubani wa shirika la WFP wametekwa Darfur. Kemal Saiki ni mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa UNAMID.

(SAUTI YA KEMAL SAIKI)

Wakati huohuo UNAMID imesema wafanyakazi watatu wa msaada wa shirika la msaada la Kikatoli waliotekwa nyara mwanzoni mwa wiki hii katika jimbo hilo wameachiliwa huru Jumatano baada ya kushikiliwa kwa siku tatu.